Mahakama ya Juu nchini Kenya, inasikiliza kesi ya dharura iliyowasilishwa siku ya Jumanne na wapiga kura watatu, wakitaka Uchaguzi mpya wa urais uliopangwa kufanyika kesho kuahirishwa kwa siku tisini.
Wapiga kura hao wanasema mazingira ya kisiasa nchini Kenya sio rafiki kuwezesha kufanyika kwa Uchaguzi utakaokuwa huru na haki.
Wakili wao Harun Ndumbi amesema ana imani Mahakamani itawapa ushindi.
“Uchaguzi huu hauwezi kufanyika na kuwa huru na haki kwa sababu ya mazingira mabaya, tunataka Mahakama ya Juu iahirishe Uchaguzi huu kwa siku tisini,” amesema Harun Ndumbi.
Jaji Mkuu David Maraga alikubali kusikiliza kesi hiyo na kuwaagiza Majaji wengine kusikiliza kesi zote kuhusu Uchaguzi hivi leo, pamoja na kwamba, leo ni siku ya mapumziko.
Kesi hii imezua wasiwasi nchini humo kuhusu hatima ya Uchaguzi wa kesho.
Wafuasi wa kiongozi wa upinzani Raila Odinga wanasubiri tangazo la kiongozi wao huku wafuasi wa chama cha Jubilee wakisema wako tayari kupiga kura.
Katika hatua nyingine, Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Wafula Chebukati, amemteua Consolata Maina kuwa Naibu msimamizi Mkuu wa Uchaguzi wa urais, uteuzi ambao umezua hisia mseto.
Naye mlinzi na dereva wa Naibu Jaji Mkuu wa Kenya Philomena Mwilu alivamiwa na watu wasiojulikana na kupigwa risasi jijini Nairobi.
Tukio hilo lilitokea baada ya mlinzi huyo kumfikisha nyumbani Naibu Jaji Mkuu huyo ambaye pia ni Jaji katika Mahakama ya Juu.
Waziri wa Usalama Fred Matiang'i amesema uchunguzi unaendelea kubaini waliotekeleza shambulizi hilo lakini akawahakikishia wafanyikazi wa Mahakama na hasa Majaji kuwa, wako salama.
No comments:
Post a Comment