Saturday, 28 October 2017

Kampuni zashindania kukuza bangi Denmark

Kampuni zashindania kukuza bangi Denmark


Kampuni nchini Denmark zimeanza kuwasilisha maombi kwa serikali kupata idhini ya kukuza bangi kujiandaa kwa wakati ambao bangi itakuwa halali nchini humo mwaka ujao.

Kampuni 13 tayari zimewasilisha maombi kwa idara ya serikali inayohusika ya Laegemiddelstyrelsen.

Bangi itakuwa halali kutumiwa kama dawa na watu wanaotatizwa na magonjwa yenye uchungu mwingi kama vile saratani na kuganda kwa misuli.

Kuanzia Januari 2018, bangi itakuwa inatolewa kama dawa kwa wagonjwa kwa majaribio ya kipindi cha miaka minne.

Gazeti la Copenhagen Post linasema kuanzia wakati huo, wagonjwa wanaweza kupendekezewa bangi kama dawa na daktari nchini humo.

Lakini bunge bado linajadiliana kuhusu mfumo utakaotumiwa.

Hilo limezifanya kampuni kubwa za kilimo cha mboga na matunda nchini humo kama vile Dansk Gartneri ya Jorgen K. Andersen kutowasilisha maombi kwa sasa.

Bw Andersen ameambia tovuti ya fyens.dk kwamba kampuni yake inatazamia kwamba kutakuwa na mkanganyiko mkubwa katika kutolewa kwa idhini ya kukuza bangi.

Baadhi ya kampuni hata hivyo zinakusudia kukuza sekta ya bangi Denmark na kuuza dawa hiyo maeneo mengine ya nje ambapo bangi ni halali.

Lars Tomassen, mkurugenzi wa Danish Cannabis anasema kwa sasa inaweza kugharimu krone 6,000 ($935; £715) kila mwezi kumtibu mgonjwa wa kawaida kwa kutumia bangi kama dawa

No comments:

Post a Comment