Thursday, 16 November 2017

Viboko 12 vyamngoja ‘bilionea’ nyumba za Lugumi


Busega. Siku moja baada ya Jeshi la Polisi kumwachia kwa dhamana, Dk Loius Shika ambaye alikuwa ameshikiliwa kwa siku sita kwa madai ya kuharibu mnada wa nyumba za Said Lugumi, familia ya daktari huyo imesema lazima achapwe viboko 12 kama anataka kusamehewa.

Akizungumza na Mwananchi nyumbani kwake katika kitongoji cha Misheni katika Kijiji cha Chamugasa juzi, kaka mkubwa wa Dk Shika, Pelanya Lunyalula alieleza kuwa mila na tamaduni za kabila la Wasukuma hazitoi msahama hivihivi hadi pale kikao cha baraza la ndugu kitakapoketi na kumpa adhabu ya viboko.

“Mpaga ibanza lya badugu (hadi kwenye kikao cha baraza la ndugu wa ukoo) wakiketi kumjadili na yeye akiwepo ndipo uamuzi hufanyika wa kumuonya kwa tabia za kudharau ukoo na huchapwa viboko zaidi ya 12 na kutakiwa kujirekebisha vingine atafutwa kabisa,” alisema.

Lunyalula alisema uamuzi huo hufanywa endapo mtu kama huyo ameamua kutengana na ndugu zake kama anavyodaiwa kufanya Dk Shika kwa madai misiba mingi imetokea na yeye kupatiwa taarifa lakini hakufika kuhani.

“Hii ni dhahiri kwamba ameona ndugu zake hawaendani na elimu yake kitendo ambacho kila mmoja alishakichukia, hivyo hata hilo suala lililomkuta huenda ni malipo ya matendo yake aliyoyafanya,” alisema Pelanya mwenye umri wa miaka 84.

Kauli hiyo iliungwa mkono na mpwa wa Dk Shika ambaye pia ni mwenyekiti wa Kitongoji cha Misheni, Emmanuel Komanya ambaye alitumia nafasi hiyo kuwaonya watu wengine wasiige tabia kama hiyo.

Ndugu hao ambao kwa pamoja walionekana kuwa na huzuni wakati wakizungumza na Mwananchi baada ya kupata taarifa za kushikiliwa kwake, walisema hawataweza kwenda kuonana naye.

“Kwanza familia yetu ni masikini hatuna uwezo wa kutafuta fedha za kwenda huko, lakini pia hata kama tungekuwa na uwezo tusingeweza kwenda (Dar es Salaam),” alisema.

Hata hivyo, Dk Shika mwenyewe alipozungumzia kuhusu familia yake hiyo alisema hawasiliani nayo kwa kuwa huenda wenzake hawana simu na hadhani kama atakwenda huko kwa kuwa wazazi wake wote wameshakufa hivyo hata akienda haitasaidia.

Juzi Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam lilifikia uamuzi wa kumwachia baada ya kutimiza masharti ya dhamana ya kujidhamini mwenyewe kutokana na kukosa mtu wa kumwekea dhamana.

Kamanda wa kanda hiyo, Lazaro Mambosasa alisema, “uchunguzi wa tuhuma dhidi yake unaendelea lakini mpaka sasa hakuna mtu yeyote aliyefika kutaka kumwekea dhamana, yaani anaishi kama mtu wa nyikani.


No comments:

Post a Comment