Saturday, 14 October 2017

Kocha Lwandamina: Vijana wapo tayari kwa kuipigania Yanga kesho

KOCHA wa Yanga, Mzambia George Lwandamina amesema kwamba wachezaji wake wako vizuri kuelekea mchezo wa kesho wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara dhidi ya wenyeji, Kagera Sugar Uwanja wa Kaitaba, Bukoba.
Akizungumza baada ya mazoezi ya jioni Uwanja wa Kaitaba, Lwandamina amesema wachezaji wake wote wapo vizuri kuelekea mchezo huo kesho jioni.
Lwandamina amesema japokuwa atawakosa wachezaji wake watatu tegemeo, Wazimbabwe kiungo Thabani Kamusoko, mshambuliaji Donald Ngoma na mshambuliaji Mrundi, Amissi Tambwe - lakini hana shaka vijana waliopo watafanya vizuri.
“Tutawakosa Kamusoko, Ngoma na Tambwe, lakini nina imani na wachezaji niliokuja nao hapa wanaweza kufanya vizuri,”amesema.
Kwa ujumla, Ligi Kuu inatarajiwa kuendelea kesho na mbali na mabingwa hao watetezi, Yanga kuwa wageni wa Kagera Sugar, Mwadui FC wataikaribisha Azam FC Uwanja wa Mwadui Complex,
Shinyanga na Ndanda watawakaribisha jirani zao, Maji Maji ya Songea Uwanja wa Nangwanda Sijaona mjini Mtwara wakati Singida United itasafiri hadi Uwanja wa Mabatini ulioko Mlandizi kucheza na wenyeji Ruvu Shooting ya Pwani.
Majirani wengine, Njombe Mji na Lipuli ya Iringa watacheza kwenye Uwanja wa Sabasaba mjini Njombe ilihali michezo mingine ya Ligi hiyo ikifanyika Jumapili Oktoba 15, ambako Simba itakuwa mwenyeji wa Mtibwa Sugar kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam wakati Tanzania Prisons itacheza na Stand United kwenye Uwanja wa Sokoine jijini Mbeya.

No comments:

Post a Comment