Saturday, 14 October 2017

Gambo: Madiwani wanakunwa na utendaji kazi wa Rais John Magufuli.

Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo amefunguka na kusema kuwa madiwani ambao wamehama kutoka CHADEMA na kuhamia CCM si kama wamenunuliwa au kuhongwa rushwa kama inavyodaiwa na baadhi ya watu bali wanakunwa na utendaji kazi wa Rais John Magufuli.
Mrisho Gambo amesema hayo leo jijini Arusha na kusema kuwa kama CHADEMA wanajiamini wanakubalika na wananchi hivyo wasubiri uchaguzi ndiyo utawapa majibu kwani anaamini kuwa Chama Cha Mapinduzi (CCM) ndiyo kitashinda nafasi hizo kutokana na kukubalika kwa wananchi.
"Wale madiwani wamekunwa na utendaji uliotukuka wa Rais John Pombe Magufuli na siyo Arusha pekee yake, kule Arumeru madiwani wametoka, Monduli wametoka na kule Ngorongoro wametoka, wao kama wanajiamini wanakubalika na wanajiamini kuwa wale watu wao wamenunuliwa lakini wao kwenye maeneo hayo wanakubalika si wasubiri si tunakwenda kwenye uchaguzi, huko hakuna uteuzi na wanaokwenda kupiga kura ni wananchi hivyo wajipange waende kusomesha watu kule" alisema Mrisho Gambo
Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mrisho Gambo ni kati ya wateule wa Rais ambao CHADEMA kupitia kwa Mbunge wa Arumeru Mashariki wanawatuhumu kuhusika na kutumia nafasi zao kununua baadhi ya madiwani wa CHADEMA kwa kigezo cha kuwa madiwani hao wanakubali kazi anazofanya Rais John Pombe Magufuli.

No comments:

Post a Comment